Site icon KahawaTungu

Wasichana Waliomkejeli Raisi Wa Burundi Kupitia Michoro Wafurushwa Shuleni

Picha ya Rais wa Burundi Pierre Nkurunziza iliyofanywa kejeli na wasichana hao. [PICHA/ KWA HISANI]

Wanafunzi watatu waliotiwa mbaroni mwezi uliopita kwa tuhuma za kumkejeli raisi wa Burundi Pierre Nkurunziza wamefushwa shuleni siku chache baada ya kuachiliwa huru.

Wasichana hao, na wengine wanne ambao waliachiliwa kwa njia tatanishi, walikamatwa kwa madai ya kumkejili raisi Nkurunziza kupitia michoro katika madaftari yao.

Kukamatwa kwa wanafunzi hao kulikashifiwa katika mitandao ya kijamii haswa Twitter kwa kutumia hashitegi #FreeOurGirls.

Wengi wanaamini kuwa mchango wao ndio uliopelekea wasichana hao wenye umri mdogo kuachiliwa.

Duru za kuaminika zinaarifu kuwa licha ya kuachiliwa mwezi uliopita kutoka gereza la Ngozi walimokuwa wamefungiwa, serikali haikutupilia mbali kesi dhidi yao.

Kulingana na shirika la kupigania haki za kibinadamu almaarufu Human Rights Watch, kesi iyo ilichangia kufurushwa kwa wasichana hao shuleni.

“Ni vizuri waliachiliwa lakini tumekuja kugundua kuwa serikali haikutupilia mbali kesi dhidi yao, watatu hao sasa wamefurushwa shuleni, ” mkurugenzi wa shirika la HRW alidokezea vyombo vya habari.

Mudge alidokeza kuwa wanafunzi hao, waliokuwa wakisomea shule ya Ecofo Akamuri iliyoko Kirundo, nchini Burundi, hawana budi ila kusalia nyumbani.

Kulingana na barua kutoka shule iyo iliyoandikwa Machi 20, wanafunzi hao walienda kinyume na sheria za masomo katika kituo hicho cha mafundisho.

“Kwa mjibu wa sheria za shule hii, kipengele cha 31 aya ya 28, wanafunzi hawa watano wamefurushwa kutoka shule hii,” barua iyo ambayo imetiwa sahihi na mkuu wa shule iyo Isaie Nkinzingabo imenukuliwa.

Soma:Burundi Yawaachilia Huru Wanafunzi Waliomkejeli Raisi Nkurunziza Kupitia Michoro

Nkinzingabo aliwaagiza wanafunzi hao kutafuta shule nyingine ili kuyaendeleza masomo yao.

Kulingana na HRW, si mara ya kwanza visa kama ivyo kushuhudiwa nchini Burundi.

Mwaka wa 2016, wanafunzi wanane wa shule ya upili walikamatwa kwa madai ya kumshurutisha raisi Nkurunziza atoke mamlakani kupitia kwa madaftari yao.

Mwaka huo huo, mamia ya wanafunzi walikamatwa kwa tuhuma za kumkashfu Rais baada ya kuchora michoro isiyofaa dhidi yake.

Watetezi wa haki za kibinadamu nchini humo wamekashifu utawala wa Rais Nkurunziza kwa wanachokitaja kuwa unyanyasaji wa haki za wanafunzi wasiokubaliana na uongozi wake.

Raisi Nkurunziza aliingia mamlakani mnamo mwaka 2005. Aliweza kuchaguliwa tena mwaka wa 2015 licha ya upinzani mkubwa kutoka kwa wananchi kwa madai ya kuzidisha kipindi chake ofisini.

Email your news TIPS to Editor@kahawatungu.com or WhatsApp +254707482874. You can also find us on Telegram through www.t.me/kahawatungu

Exit mobile version